FIFA kumlipa mlinda mlango wa Togo

Mlinda mlango wa Togo aliyejeruhiwa Kodjovi Obilale amesema anatazamia kulipwa na Fifa dola za Marekani 25,000 baada ya kupigwa risasi mwezi Januari wakati timu hiyo ikielekea Angola kwa fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Image caption Kodjobi Obilale

Obilale, mwenye umri wa 25, bado hawezi kutembea ikiwa imepita miezi minane baada ya shambulio la risasi la waasi wanaotaka kujitenga na jimbo la Cabinda lililoelekezwa kwenye basi la wachezaji wa Togo walipokuwa wakiingia Angola.

Watu wengine wawili waliokuwemo katika msafara wa timu ya Togo waliuawa, huku mlinda mlango wa akiba alipigwa risasi mara mbili mgongoni.

Obilale amesema "huo ni wema" baada ya kupokea barua kutoka kwa Rais wa Fifa, Sepp Blatter.

Akiwa amekatishwa tamaa kukosa msaada wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) pamoja na waandalizi wa mashindano hayo nchi ya Angola, Obilale alimuandikia barua Blatter mwezi wa Agosti akimuomba msaada.

Blatter alimuahidi msaada kutoka mfuko wa FIFA wa huduma za kibinadamu, licha ya kusema Shirikisho hilo lisibebeshwe lawama kutokana na shambulio la Kabinda.

Blatter ameandika barua akisema "Tutaendelea kuchunguza tukio," Na kuongeza "Nakutakia uwe na ujasiri mkubwa."

Obilale ametoa lawama zake hadharani kwa kukosa msaada wa CAF na maafisa wa Angolan baada ya shambulio ambao limemfanya asiweze tena kucheza soka.

Mlinda mlango huyo aliyekuwa akichezea klabu moja ya ngazi ya chini nchini Ufaransa, hawezi kuinua mguu wake wa kuume chini ya goti na pia miguu yake imekufa ganzi, lakini ana matumaini makubwa ataweza kutembea siku zijazo.

Akiwa anatumia kiti maalum cha kutembelea, Obilale amesema kama jina lake lingekuwa kubwa, basi matibabu yake yangekuwa tofauti na anayopata sasa.

Obilale, ambaye kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu ya utaalamu wa mamacheza, wa kufanyiwa mazoezi ya viungo vyake kila siku, alifarijika baada ya kupokea msaada kutoka sehemu nyingine tofauti.

Aliahidiwa malipo ya dola 70,000 na Waziri wa Michezo wa Togo mwezi uliopita na fedha hizo ziliingia katika akaunti yake wiki hii.

Mlinda mlango huyo amesema pesa hizo zitamsaidia kwa matibabu ya miezi mitatu tu kati ya saba anayodaiwa hospitalini.

Anakusudia kupeleka ankara ya matibabu iliyosalia kwa serikali ya Togo.