Chelsea na Arsenal zapeta Ubingwa Ulaya

Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti amesisitiza wachezaji wake waliweka kando matatizo yao ya hivi karibuni na kufanikiwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya Marseille katika ligi ya Ubingwa wa Ulaya.

Image caption Wachezaji wa Chelsea wakishangilia

Amesema ana matumaini wapo katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua inayofuata.

Ancelotti amezidi kujigamba kwamba Chelsea ipo katika hali nzuri, wakiongoza kundi lao na hali kadhalika wakishikilia usukani wa Ligi Kuu ya England.

Nao Arsenal wakiwa wanacheza ugenini waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Partizan Belgrade waliokuwa wakicheza pungufu ya mchezaji mmoja.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, anaamini mlinda mlango Lukasz Fabianski atazidi kujiamini kutokana na jinsi alivyodaka vizuri katika mchezo huo.

Fabianski anayefahamika zaidi kwa kucheza ovyo akiwa na Arsenal, alionekana mwenye kujiamini na akapangua mkwaju wa penalti katika pambano hilo la Ubingwa wa Ulaya kundi H.

Hata hivyo, Wenger alisita kuthibitisha iwapo Fabianski, aliyecheza badala ya mlinda mlango namba moja Manuel Almunia, aliyejeruhiwa kiwiko cha mkono, kama atachaguliwa kulinda lango siku ya Jumapili dhidi ya Chelsea.