Jumuiya ya Madola 2010 India

Image caption Kazi ikiendelea katika uwanja wa michezo wa Nehru mjini Delhi

Mashindano haya ya 19 yatafanyika India kwa mara ya kwanza na ni mara ya pili kwa mashindano ya Jumuia ya Madola kufanyika katika Bara Asia.

Mara ya kwanza yalifanyika katika mji wa Kuala Lumpur mwaka 1998.

Mji wa Delhi ulishinda kinyang'anyiro cha kuandaa mashindano ya mwaka huu wa 2010 baada ya kushinda kura za wajumbe 46 dhidi ya kura 22 za mji wa Hamilton, Canada kwenye mkutano mkuu wa shirikisho la michezo ya jumuia ya madola uliokutana mjini Montego Bay Jamaica mwezi Novemba mwaka 2003.

Tangu hapo India ikaonyesha moyo wa kuweza kujiandaa vilivyo kwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2010.

Ishara hizi zilijitokeza kwenye mashindano ya 18 mjini Melbourne, Australia mwaka 2006 iliposhiriki mashindano ambayo si kawaida kwa wanariadha wake kushiriki mbio fupi kama mita 100, 200, 400 na hata 800.

Ujumbe wa India ulikuwa mkubwa kwenye mashindano hayo na katika hotuba za mjumbe wa India wakati wa sherehe za kuhitimisha mashindano ya Melbourne, aliahidi kuwa India itawakaribisha wanariadha na familia ya Jumuia ya madola kwa kishindo mjini New Delhi miaka minne kuanzia wakati huo.

Mwaka 2010 miaka minne baadaye, na mwezi mmoja kabla ya mashindano kuanza, habari zikajitokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa mashindano hayo yasifanyike kutokana na kuchelewa kwa vifaa kama malazi ya wanariadha na kadhalika.

Image caption Uwanja wa michezo wa Jumuiya ya Madola

Waziri wa India wa maendeleo ya vijijini, Jaipai Reddy alijibu shutuma hizo kwa kusema kuwa vyombo vya habari vimetia chumvi matayarisho hayo na kukanusha kuwa kuna tatizo katika vyumba vya wanariadha.

Kuna maoni tofauti lakini tumefikia hatua ya kuridhisha ila tu, usafi wa vyumba vya wanariadha. Tutatumia kila mbinu, kila njia, tutaajiri wafanyakazi wengi kusafisha vyumba hivyo na mnamo saa 48 kila kitu kitakuwa sawa sawa.

Ahadi ya waziri huyo ilipokelewa vyema ingawa athari za taarifa za habari zilikuwa tayari zimesababisha baadhi ya wanariadha maarufu kuamua kujiondoa.

Hata hivyo wajumbe wa Afrika kwenye halmashauri ya shirikisho la michezo ya jumuia ya madola walikwenda kuchunguza na kushiriki kwenye vikao kuonakila juhudi inafanyika kuondoa hali hiyo ya mtafaruku. Steven Soyi ni mjumbe wa Kenya kwenye mashindano haya.

Baada ya wiki moja ya kuajiri watumishi zaidi, mafundi na wasaidizi, waziri wa India Jaipul Reddy alisema maandalizi kwa sasa ni muruwa. Hakuna sababu ya kutishika.

Waziri Reddy alisema hana wasiwasi kuhusu maandalizi. Alisema kuwa kuna mashaka juu ya viwango vya usafi wa vyoo katika kijiji cha wanariadha. Mbali na hayo haoni tatizo lolote.

Inasemekana wanariadha wa England, Scotland, Wales, Australia, Rwanda, Uganda na Kenya tayari wamo ndani ya kijiji cha michezo na wameanza mazoezi kwenye viwanja ambako mashindano yatafanyika kuanzia Jumapili tareh 3 Oktoba.

Na habari hivi karibuni kutoka Delhi zinasema kuwa wakosoaji wengi wamebadili hisia na sasa wanasubiri kwa hamu mashindano ambayo yanaweza kuvunja rekodi ya kuwa murua kuliko mengine ya Jumuia ya Madola.