Benki kuu ya Kenya kuchunguza "Hawala"

Image caption Pesa za mahawala

Kenya imetangaza mipango inayonuia kudhibiti ufadhili wa kifedha unaotolewa kwa wapiganaji wa kiisilamu wa Al- Shabaab nchini Somalia.

Benki Kuu ya Kenya imeziagiza benki zote nchini kuchunguza shughuli za kibiashara zinazohusishwa na wafanyibiashara walioorodheshwa kama wafadhili wa ugaidi na Umoja wa Mataifa.

Ugaidi

Hatua ya Kenya katika kujaribu, kupunguza nguvu za wanamgambo wa Ki-Somali inatokea wiki moja baada ya baraza la usalama la umoja wa Mataifa kufanya kikao maalum kilichoangazia hali ya Somalia.

Wadadisi wa mambo ya usalama wamekuwa wakisisitiza kwamba Nairobi imekuwa kivukishio cha ufadhili wa makundi yanayokabiliana na serikali ya mpito ya somalia.

Moja ya njia zinazotumiwa na wasomali kuwatumia jamaa zao fedha ni Hawala.

Maoni

Hata hivyo mahawala hao wametetea biashara yao wakisema kuwa wanafanya uhalali usiovunja sheria za nchi.

Hussein Mohammed Haji ni naibu mwenyekiti wa wafanyibiashara wasomali jijini Nairobi: " hii Hawala ni kama amana ambayo mtu anapewa pesa mahali moja na analpiwa mahali pengine. Mtu anasema tu anataka kutuma pesa mahali fulani na mara moja anapeana jina lake, namba ya simu na mara moja inafanyika"

Kunao wale wanaosema kuwa hili ni jambo la kitamaduni na wala sio kisheria.

Simiyu Werunga ni mdadisi wa masuala ya Kiusalama nchini Kenya. "Kisheria sio halali, lakini ni kitu cha utamaduni. Na wakati mwingine watu hawapendelei kuingilia mambo ya utamaduni kwasababu ni kitu kimefanyika kwa wakati mrefu. Ni kama zamani tulitumia mambo ya 'Barter Trade'. Japo haikupigwa marufuku, pesa zilikuja na barter trade ikaisha yenyewe. Iliachwa kuendelea kwasababu ilisaidia watu".