Drogba akanusha kuiacha Ivory Coast

Nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast Didier Drogba, amekanusha taarifa zilizozagaa kwamba amestaafu kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo.

Vyombo vingi vya habari vya Ivory Coast vimedai nyota huyo wa Chelsea ameiacha timu ya taifa baada ya kutocheza mchezo wa kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32 hakucheza pambano la mwezi Agosti ambapo Ivory Coast iliifunga Rwanda na pia hatakuwemo katika kikosi cha timu ya taifa kitakachosafiri kwenda Burundi wiki ijayo.

Drogba amesema hafahamu kwa nini taarifa hizo zimesambaa.

Alisema alikuwa anapumzika tu baada ya kufanyiwa upasuaji mara mbili kwa kipindi chini miezi miwili. Kwa hiyo alikuwa akihitaji kurejesha hali yake iwe ya kawaida kimchezo.

"Iwapo meneja ataniita kwa mchezo ujao, basi sitasita kupanda ndege kuitetea nchi yangu." Ameongeza Drogba.

Mwezi wa Juni, Drogba alifanyiwa upasuaji wa dharura wa kiwiko cha mkono ili aweze kucheza katika Kombe la Dunia, baada ya kuvunjika katika mechi ya kirafiki ya maandalizi dhidi ya Korea Kusini.

Aliruhusiwa na Fifa kuvaa kifaa maalumu cha kumkinga katika mashindano ya kwanza ya Kombe la Dunia kufanyika Afrika na aliweza kucheza mechi zote tatu, akafunga mara moja, lakini hakuweza kuizuia Ivory Coast isitolewe katika hatua ya awali nchini Afrika Kusini.

Baada ya mchezo wa wiki ijayo wa kundi H mjini Bujumbura, tembo hao wa Ivory Coast hawatacheza hadi mwezi wa Machi mwakani.

Drogba ndiye mfungaji bora kwa timu yake ya taifa katika historia ya nchi yake, ambapo ameifungia mabao 45 hadi sasa.