Matokeo ya Ligi ya England Jumamosi

Everton imeweza kupata pointi tatu muhimu ugenini baada ya kuwalaza wenyeji wao Birmingham kwa mabao 2-0 na kujinasua kutoka timu tatu zilizokuwa zikishikilia mkia. Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa Everton msimu huu. Kwa ushindi huo Everton ilifuta rekodi ya Birmingham ya kutopoteza michezo 18 ya nyumbani.

Image caption Matokeo ya Ligi Kuu ya England

Mabao ya Everton yalifungwa katika kipindi cha pili na Roger Johnson katika dakika ya 54 na Tim Cahill dakika za nyongeza kipindi cha pili. Kwa ushindi huo Everton imefikisha pointi sita na inashikilia nafasi ya 17.

Nae Jon Walters aliweza kufunga bao lake la kwanza kwa Stoke wakati timu hiyo ilipopata ushindi wa nyumbani dhidi ya Blackburn Rovers. Kwa matokeo hayo Stoke City imepanda hadi nafasi ya saba wakiwa na pointi 10.

Rafael Van der Vaart aliipatia ushindi muhimu Tottenham baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya moja la Aston Villa. Aston Villa ndio walikuwa wa kwanza kuliona lango la Tottenham baada ya kazi nzuri ya Emile Heskey aliyemtoka Sebastian Bassong na kuachia krosi iliyowekwa kimiani na Marc Albrighton. Tottenham kwa ushindi huo wamepanda hadi nafasi ya tano wakiwa na pointi 11.

West Bromich walikwenda sare ya kufungana bao 1-1 na kugawana pointi, huku West Ham nao waliweza kujikakamua na kutoka sare ya bao 1-1 na Fulham.

Nao Manchester United wakicheza ugenini na Sunderland hawakuweza kufurukuta na kugawana pointi katika mchezo ambao timu hizo hazikuweza kufungana. Kwa matokeo hayo bado Manchester United wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na pointi 13 na Sunderland wakiwa na pointi nane wakishika nafasi ya 10.

Katika mchezo uliochezwa mchana Wigan waliutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kuwalaza Wolves mabao 2-0 na kujinyanyua hadi nafasi ya 13 wakiwa na pointi nane. mabao ya Wigan yalipachikwa na Jordi Gomez na Hugo Rodallega.