Ataka apatiwe nafasi zaidi kucheza

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney anaamini ni vyema apatiwe nafasi ya kucheza ili arejesha kiwango chake cha soka.

Image caption Wayne Rooney

Rooney mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akikabiliwa na hali ngumu ya kushuka kiwango chake pamoja na tumuha za maisha yake binafsi lakini akajitetea kwa kusisitiza; "Mimi ni binadamu tu wa kawaida."

Mshambuliaji huyo kwa sasa hachezi kutokana na kuumia kiwiko cha mguu, ingawa ana matumaini atakuwa amepona kuikabili Montenegro tarehe 12 mwezi huu wa Oktoba kwa pambano la kufuzu Ubingwa wa Ulaya mwaka 2012.

Amesema: "Nahitaji kumaliza matatizo haya na kurejea kucheza soka katika kiwango changu cha kawaida."

Rooney ambaye hajaifungia bao Manchester United katika michezo ya awali msimu huu, aliondolewa katika kikosi cha timu hiyo kilichopambana na klabu yake ya zamani Everton baada ya tuhuma za maisha yake binafsi.

Baada ya kujeruhiwa katika kipindi cha pili cha pambano dhidi ya Bolton ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 hivi karibuni, meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson alimuacha mshambuliaji kucheza pambano la Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Valencia.

Kuumia kwake pia kumemfanya akose mechi ya ligi ya England dhidi ya Sunderland.

Lakini Rooney, ambaye anaweza kuwemo katika kikosi cha England siku ya Jumatatu kitakachopambana na Montenegro, anaamini kucheza mara kwa mara ndio dawa pekee ya yeye kuinua kiwango chake.

Amesema; Mimi ni binadamu kama wengine, naumia pia. Najua naweza kucheza vizuri, kwa hiyo natumai nikicheza mara kwa mara katika timu yangu, naamini kiwango changu kitarejea kama ilivyokuwa siku za nyuma."

Ferguson bado anasita kurejesha Rooney haraka uwanjani, ingawa anaamini mshambuliaji huyo ataweza kucheza pambano dhidi ya Montenegro na uamuzi huo anamuachia kocha wa England Fabio Capello.