Chelsea yashinda, Liverpool yapoteza

Chelsea imezidi kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya soka ya England kwa kuweka wigo wa pointi nne kwa magoli yaliyofungwana na Didier Drogba na Alex yaliyowapatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal.

Image caption Wachezaji wa Chelsea wakishangilia

Drogba alipachika bao la kwanza kwa kisigino baada ya kuunganisha krosi ya Ashley Cole katika nafasi iliyoonekana vigumu kufunga lakini mpira ukajaa wavuni katika kipindi cha kwanza.

Na Alex akashindilia msumari wa mwisho kwa Arsenal alipopachika bao la pili kwa shuti kali la adhabu ndogo lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Arsenal walikuwa na muda wa kumiliki mpira lakini ni mara chache waliweza kumjaribu mlinda mlango wa Chelsea Petr Cech, ambaye aliokoa mkwaju mkali wa Andrey Arshavin dakika za mwanzo.

Kwa matokeo hayo Chelsea wanaendelea kuongoza wakiwa na pointi 18.

Nayo Blackpool ikicheza soka ya kupendeza ugenini katika uwanja wa Anfield ilizidi kuongeza machungu kwa timu ya Liverpool kwa kuwalaza mabao 2-1.

Charlie Adam wa Blackpool alikuwa wa kwanza kupatia bao kwa mkwaju wa penalti baada ya Glen Johnson kumkwatua Luke Varney.

Liverpool walisawazisha kwa bao lililofungwa kwa kichwa cha nguvu kilichopigwa na Sotirios Kyrgiakos na nusura asawazishe katika dakika za nyongeza lakini kazi nzuri iliyofanywa na Matt Gilks iliikosesha Liverpool nafasi.

Kufungwa huko kwa Liverpool kumezidi kuweka giza kwa timu hiyo ambayo pia imekwishatolewa katika mbio za kuwania kombe la Carling Cup na klabu ya Ligi ya daraja la pili Northampton na sasa wapo nafasi ya tatu kutoka chini ya msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Na katika mchezo wa mapema Manchester City pamoja na kutocheza vizuri walipigana kiume na kufanikiwa kuzoa pointi tatu dhidi ya Newcastle kwa kuwafunga mabao 2-1 na kupanda hadi nafasi ya pili.

City waliweza kupata bao la kwanza lililofungwa na Carlos Tevez kwa mkwaju wa penalti baada ya Mike Williamson kumchezea rafu.

Lakini Newcastle, walisawazisha kwa bao lililofungwa na kwa shuti la karibu na Jonas Gutierrez.

Adam Johnson aliyeingia mchezaji wa akiba aliipatia City bao la pili.

Ushindi huo umeichukua City hadi nafasi ya pili nyuma ya Chelsea..