Sven-Goran Eriksson meneja Leicester

Sven-Goran Eriksson amechaguliwa kuwa kocha meneja mpya wa Leicester City baada ya kutangazwa rasmi na klabu hiyo siku ya Jumapili.

Image caption Sven-Goran Eriksson

Meneja huyo wa zamani wa England anachukua nafasi ya Paulo Sousa, aliyetimuliwa siku ya Ijumaa huku timu hiyo ikiwa nafasi tatu za mwisho baada ya kucheza mechi tisa.

Eriksson, mwenye umri wa miaka 62, ameingia mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.

Amesema katika mkutano na waandishi wa habari:" Nina furaha kuwa hapa. Klabu inataka kupanda daraja kucheza Ligi Kuu nami pia nahitaji iwe hivyo. Hilo ni lengo ambalo lipo wazi."

Meneja huyo raia wa Sweden alikuwa akitazama pambano katika uwanja wa Walkers ambapo klabu yake hiyo mpya iliifunga Scunthorpe mabao 3-1 siku ya Jumamosi na siku ya Jumapili meneja huyo wa zamani wa Manchester City alifahamisha ameridhika na kiwango cha timu yake mpya.

Eriksson amekuwa hana timu ya kufundisha tangu alipoingoza Ivory Coast katika fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, ambako alishindwa kuipeleka timu hiyo katika hatua ya mtoano.

Mbali na hilo Eriksson aliwahi kwa miezi saba kushika wadhifa wa Ukurugenzi wa soka katika klabu ya Notts County na pia mwezi Juni mwaka 2008 hadi Aprili mwaka 2009 alikuwa meneja wa timu ya taifa ya Mexico.

Leicester, ambayo hivi karibuni ilichukuliwa na kampuni ya Thailand, ilifika hatua ya kucheza nusu fainali msimu uliopita Ligi ya Championship chini ya Nigel Pearson, ambaye baadae aliondoka na kujiunga na klabu ya Hull City.