Hodgson ana wasiwasi na Liverpool

Roy Hodgson
Image caption Roy Hodgson

Meneja wa Liverpool Roy Hodgson amekiri timu yake imeingia katika hekaheka ya kujinasua katika wimbi la kushuka daraja, lakini akasema ana wasiwasi zaidi na kiwango cha baadhi ya wachezaji wake.

Liverpool walifungwa mabao 2-1 na Blackpool katika uwanja wao wa Anfield na kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Hodgson amesema: "Imesalia michezo 31 lakini unapokuwa katika eneo la kushuka daraja basi unakabiliwa na vita ya kujikwamua."

"Lakini hofu yangu sidhani ipo katika eneo la kushuka daraja, ila ni kiwango cha wachezaji."

Alipoulizwa iwapo pointi sita walizonazo kibindoni kutokana na michezo saba waliyocheza kama zinawatia wasiwasi, Hodgson alijibu: "Bila shaka ndio. Hii ni Liverpool. Ni klabu kubwa na timu kubwa na hakuna hata mmoja kati yetu anakayekubali hali hii.

"Hatuwezi kufanya lolote kuhusiana na hali hii kwa sasa lakini hatuna budi kujituma zaidi katika mechi zinazofuata."

Liverpool ilifungwa bao la kwanza la mkwaju wa penalti wa Charlie Adam na bao la pili likapachikwa na Luke Varney na licha ya kucheza vizuri kipindi cha pili ilifanikiwa tu kupata bao la kufutia machozi lililopachikwa na Sotirios Kyrgiakos.

Kuanza kusuasua kwa Liverpool msimu huu, hali inayoonekana ni mbaya tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya England, kumeshuhudiwa timu hiyo ikitolewa mapema katika heka heka za kuwania Kombe la Carling ilipofungwa nyumbani na klabu ya daraja la pili ya Northampton.

Hodgson pia alikabiliana na kelele za mashabiki waliokuwa wakipaza sauti wakitaja jina la Kenny Dalglish wakati wa mechi ya Jumapili. Dalgish mchezaji wa zamani wa Liverpool, kwa sasa anashikilia nafasi ya ubalozi ndani ya klabu hiyo, inasemekana alikuwa tayari kuchukua nafasi ya umeneja kabla ya kuteuliwa kwa Hodgson.

Dalglish alikuwepo uwanjani na alishuhudia timu yake ikizomewa mwishoni mwa mchezo.

Laknini mshambuliaji wa Liverpool Dirk Kuyt ana matumaini wachezaji wanaweza kubadili hali ya mambo ilivyo kwa sasa.