Waalgeria wawili 'hawakufungua Ramadhan'

Image caption Waislamu wakiswali wakati wa Ramadhan, Algiers

Wakristo wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kuvunja sheria za kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan nchini Algeria wamefutiwa makosa yao.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yalisema kesi hiyo ilikuwa ni ukiukwaji wa haki ya kuabudu kulingana na katiba.

Hocine Hocini na Salem Fellak walikamatwa mwezi Agosti wakati wa Ramadhan, baada ya kuonekana wakila chakula cha mchana katika jengo walilokuwa wakifanyia kazi huko Kabylie, kaskazini mwa Algeria.

Wakili wa watu hao wameita uamuzi huo "ushindi wa haki".

Keshi nyingine mbili kama hizi zinatarajiwa kusikilizwa katika wiki za hivi karibuni.

Algeria ni nchi yenye Waislamu wengi zaidi; Wizara ya masuala ya kidini inakadiria kuwa kuna takriban Wakristo 11,000 tu miongoni mwa watu milioni 36 nchini humo.

Adhabu ya mpaka miezi mitatu jela nchini Algeria hutolewa kwa kufungua wakati wa Ramadhan.

Idadi kubwa ya Wakristo Algeria ni wa madhehebu ya Kiprotestant.