Barua za Mandela zaelezea usumbufu jela

Barua zilizoandikwa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela wakati alipokuwa miaka 27 gerezani zinaeleza maumivu makali aliyokuwa akiyasikia alipotenganishwa na familia yake.

Dondoo za barua hizo, zitakozoanza kuuzwa siku ya Jumanne, zinaonyesha jinsi alivyokuwa tafrani wakati mke na watoto wake walipokuwa wakisumbuliwa na serikali ya ubaguzi wa rangi.

Alimwambia Winnie Mandela alipotumikia kifungo cha miezi 18 alipotengwa na kufungiwa katika chumba cha peke yake, " Najihisi nimelowanishwa kwenye kidonda."

Katika barua kwa watoto wake aliandika, "Kwa muda mrefu mnaweza kuishi kama yatima."

Image caption Nelson Mandela

Nakala za barua nyingi zilikuwa zikiandikwa katika madafatri ambayo yalitaifishwa na serikali.

Hatimaye zilirejeshwa kwake na aliyekuwa askari wa usalama mwaka 2004.

Mwandishi wa kujitegemea anaelezea namna mume na mke, wanavyojaribu kushikilia familia yao pamoja huku kukiwa na mtikisiko mkubwa wa kisiasa na hisia.

Mwaka 1969, aliwaandikia mabinti zake wawili, Zeni na Zindzi wenye umri wa miaka tisa na 10, wakati wote wawili yeye na mkewe wakiwa gerezani.

Aliwaambia, " Sasa hamtosherehekea siku za kuzaliwa wala Krismasi, hamna zawadi au magauni mapya hamna viatu wala vidude vya kuchezea watoto."

Katika mwaka huo huo, alizuiwa kuhudhuria mazishi ya Thembi, mtoto mkubwa wa kiume miongoni mwa watoto wake wawili katika ndoa ya mwanzo, aliyefariki dunia kwenye ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 24.

Aliandika, " Nilipoambiwa kwa mara ya kwanza kuhusu kifo cha mwanangu nilitikisika tangu juu mpaka chini."

Barua kwa Winnie Mandela mwezi Agosti 1970 inaonyesya hasira kutokana na misukosuko inayoikumba familia yake.

Uhusiano uliojaa wasiwasi

Barua hizo pia zinaonyesha uhusiano wake na Winnie Mandela. Mwaka 1976 aliandika kwamba tatizo lake kubwa ni "kulala bila wewe kuwa pembeni mwangu na kuamka bila wewe kuwa karibu yangu, kupita siku bila mimi kukuona wewe."

Wakati huo, alipandishwa cheo na chama cha African National Congress kama ishara ya ya kupambana kwake na ubaguzi wa rangi. Lakini katika miaka ya kati ya 80 matendo yake yaliongezeka kuwa na utata na uhusiano wao ulianza kuleta wasiwasi.

Image caption Nelson na Winnie Mandela

Mwaka 1987, aliandika kwa rafiki yake kuhusu hasira aliyoonyesha Winnie Mandela alipomwambia namna watoto wake wawili wa kike walivyokuwa wakubwa: "Alinikumbusha:Mimi, si wewe, ndiye niliyewakuza hawa watoto ambao sasa unanileza mimi. Nilishtushwa."

Japokuwa alitembea naye sambamba alipoachiwa huru mwaka 1990, walitengana mwaka 1992 na kuachana miaka minne ijayo.

Aya kutoka barua hizo zimetolewa kwenye gazeti la Uingereza, The Sunday Times, na katika magazeti ya Afrika Kusini.

Zimechapishwa kwenye kitabu, Mazungumzo na Nafsi yangu, inayojumuisha hifadhi za nyaraka za kumbukumbu na vitu alivyorekodi mwenyewe pamoja na barua.

Kutoka dondoo moja kwenye kitabu hicho, ni wazi kuwa Bw Mandela alianza kuwa mwangalifu kutokana na kuongezeka kwa heshima yake katika nyanja za kimataifa wakati alipokuwa gerezani katika kisiwa cha Robben.

"Jambo moja ambalo lilikuwa likinitia wasiwasi mno ni sura isiyo sahihi nilioiweka bila kujua kwa ulimwengu wa nje; wa kuonekana kama mtakatifu.

"Sijawahi kuwa hivyo," Aliandika