Wanawake wa Kenya wang'ara New Delhi

Kenya ilizoa medali zote katika mbio za wanawake mita 5,000. Bingwa wa dunia Vivian Cheruiyot alishinda katika muda wa 15:55.12 akifuatiwa na Sylvia Kibet aliyenyakua medali ya fedha huku Ines Chenonge akipata shaba.

Silas Kiplagat wa Kenya alishinda mbio za wanaume mita 1,500 katika muda wa 3:41.78, na mwenzake James Magut akashika nafasi ya pili . Lakini bingwa mtetezi Nick Willis wa New Zealand amewazuia Wakenya kupata ushindi wa nafasi zote tatu kwa kupata shaba.

Katika mashindano ya kupokezana vijiti za mita 400 upande wa wanaume, Australia imenyakua dhahabu katika muda wa 3:03.30, ikifuatiwa na Kenya na Uingereza ikashinda shaba nyingine katika muda wa 3:03:97.

England imezoa medali za dhahabu katika mbio za mita 400 za kupokezana vijiti, wakishinda mashindano yote ya wanaume na wanawake iliyompa Mark Lewis-Francis medali yake ya pili katika kipindi cha wiki moja.

India nayo ilishangaza wengi kwa kushinda mbio za mita 400 za kupokezana vijiti siku ya Jumanne katika mashindano ya Jumuiya ya Madola, huku Ashwini Akkunji akimpiku mpinzani wa Nigeria muda kodogo tu kabla ya kufika mwisho huku Mandeep Kaur akishinda.

Dhahabu hiyo ni ya pili tu katika historia ya mashindano hayo kwa India. Mhindi mwengine pekee mwanariadaha aliyeshinda medali katika mashindano hayo ni Milkha Singh. Alinyakua dhahabu mwaka 1958 huko Cardiff, Wales.