Capello asema England haijakata tamaa

Meneja wa England Fabio Capello ameahidi kuendelea kupambana licha ya kikosi chake kubanwa na Montenegro na kutoka sare ya kutofungana katika mechi ya kuwania kufuzu Ulaya mwaka 2012.

Image caption Fabio Capello

England ilimiliki mchezo kwa muda mrefu katika uwanja wa Wembley, lakini walitafuta nafasi chache zilizowapa shida kuipenya ngome imara ya wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo England inaendelea kushikilia nafasi ya pili katika kundi lao la G, wakiwa pointi tatu nyuma ya Montenegro wakiwa na mchezo mmoja zaidi, lakini Capello amesema: "Mimi ni mpiganaji. Ni mchezo mmoja.

"Nadhani kikosi chetu ni imara, lakini mlinda mlango wao alicheza vizuri. Hii ni soka."

Mlinda mlango wa Montenegro Mladen Bozovic aliokoa kwa ustadi mikwaju miwili mmoja wa Wayne Rooney na mwengine wa karibu wa Gareth Barry.

Lakini kwa ujumla England ilishindwa kuipenya ngome imara ya Montenegro, huku washambuliaji wa pembeni Adam Johnson na Ashley Young walizimwa kabisa na safu ya ushambuliaji wa kati Rooney na Peter Crouch, na baadae Kevin Davies, hawakufurukuta.

Wenyeji nusura wapachikwe bao baada ya Milan Jovanovic kupiga shuti la kiufundi lililompita mlinda mlango wa England Joe Hart zikiwa zimesalia dakika saba, lakini shuti liligonga mwamba juu wa lango.

Capello alishindwa kujizuia kukisifu kikosi cha Montenegro kinachofundishwa na Zlatko Kranjcar jinsi kilivyokuwa kikicheza kwa kujiamini na kwa utulivu.