Owen Hargreaves kurejea uwanjani

Owen Hargreaves anajiandaa kurejea uwanjani katika kikosi cha Manchester United baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuumia na huenda akacheza siku ya Jumamosi dhidi ya West Brom katika pambano la Ligi Kuu ya England.

Image caption Owen Hargreaves

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 hajaanza kucheza mechi yoyote tangu mwezi wa Septemba mwaka 2008 kutokana na tatizo sugu la maumivu ya goti.

Kwa mujibu wa daktari Richard Steadman aliyekuwa akimtibu "Owen anatakiwa kucheza kwa kipindi fulani katika mechi ya Jumamosi."

Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alifanyiwa upasuaji wa magoti yake yote mawili katika kliniki ya daktari Steadman huko Vail, Colorado, mwaka 2008 na alikuwa akipata shida kupona haraka.

Hargreaves mara ya mwisho aliichezea Manchester United mwezi wa Mei, kwa dakika tatu za mwisho za mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Sunderland.

Mchezaji huyo alitarajiwa kuwa amepona kabisa tayari kuanza mechi mbalimbali mwanzoni mwa msimu huu, lakini alipata matatizo mengine ya goti na aliwajibika kurejea kwa Steadman huko Colorado kwa matibabu zaidi.

Hargreaves alijiunga na Manchester United mwezi Julai mwaka 2007 akitokea Bayern Munich, lakini mechi yake ya mwisho kucheza kikamilifu ilikuwa ni dhidi ya Chelsea mwezi wa Septemba mwaka 2008 walipotoka sare ya bao 1-1.