Uefa yachunguza fujo mashabiki wa Serbia

Shirikisho la soka barani Ulaya-Uefa limeanza kuchunguza ghasia zilizofanywa na mashabiki wa Serbia zilizosababisha mchezo wao na Italia wa kufuzu mashindano ya Euro 2012 kuvunjika.

Image caption Michel Platini

Vurugu zilizotokea kabla ya mchezo mjini Genoa awali zilisababisha mchezo huo kuchelewa kuanza, kabla ya kuvunjwa baada ya kuchezwa kwa dakika sita tu.

Ripoti za mwamuzi wa mchezo huo na kamisaa zitajadiliwa katika uchunguzi huo.

Miongoni mwa adhabu ambazo Uefa zinaweza kutoa ni pamoja na kufungiwa ama faini, uwanja kufungwa ama hata timu kuondolewa katika mashindano yanayoendelea au yajayo.

Mkuu wa Chama cha Soka cha Serbia Tomislav Karadzic amesema kulikuwa na dalili za kutokea ghasia, ambazo amesema " zimetuudhi na kutuletea aibu nchini kwetu.""

Mashabiki hao ilionekana walijiandaa. Ilionekana huenda wangefanya kila wawezalo kuvuruga mchezo huo usifanyike.

Karadzic amekiambia kituo kimoja cha televisheni ya Belgrade B92, ghasia hizo zilipangwa tangu nyumbani, huku mashabiki waliosafiri wakiwa wamejiandaa kutekeleza fujo kwa njia yoyote ile.

Ameongeza kusema: "Tulikuwa na matatizo wakati wa mazoezi, kabla ya mechi na sasa yametokea haya. Nchi lazima itoe tamko."

Italia, ambayo ilitolewa kwa aibu katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Afrika Kusini wakiwa mabingwa watetezi, ilikuwa na pointi saba kutokana na michezo yake mitatu ya ufunguzi, ambapo Serbia ilikuwa na pointi tatu baada ya kufungwa na Estonia Ijumaa iliyopita.