Mashindano ya Jumuiya ya Madola yamalizika

Image caption John Kelai, Kenya

John Kelai na Irene Jerotich walihitimisha kiu ya Kenya kwa kuipatia medali mbili za dhahabu katika siku ya mwisho ya mashindano ya Jumuia ya Madola ya mara ya 19 New Delhi.

Kelai alivuta kasi mbio katika mbio za marathon zilipofikia kati akimaliza katika muda wa saa 2 dakika 14 na sekunde 35, akifuatiwa na Michael Shelley wa Australia aliyempita Matui Tirop kuinyakulia Australia medali ya fedha na Tirop kuridhika na shaba.

Katika mbiio za wanawake Irene Jerotich alimuacha mwenzake Irene Mogake baada ya wakimbiaji hao kwenda sambamba kwa kipindi kirefu wakipeana mawaidha lakini hatua ya kutimka ilipowadia Jerotich akaonyesha tofauti baina yao akimaliza mbio katika muda wa saa 2 dakika 34 na sekunde 32.

Mogake alimaliza wa pili akimuachia Lisa Weighman wa Australia shaba.

Ushindi wa Jerotich haukushangaza wengi wakimtarajia kufanya vyema kwenye mashindano haya baada ya kuweka muda bora msimu huu wa mashindano ya marathon duniani.

Katika hali ya hewa yenye joto kali bila upepo mzuri Jerotich ameonyesha kuwa mwenye kasi na ustadi katika hatua ya mwisho ya kilomita mbili kufikia uzi wa kumalizia.

Mapema katika mbio hizi Jerotich alidondoka kwenye meza iliyowekewa vinywaji vya wakimbiaji ikitishia kuathiri mbio hizi na kuleta hofu kuwa huenda akaishia hapo lakini aliinuka na kuendelea na mbio hadi kutangulia mwisho wa mashindano na kuiongezea Kenya medali nyingine ya dhahabu.

Kwa kipindi kirefu cha mbio hizi Beata Naigambo alionyesha kama anayeweza kuibuka mmojawapo wa washindi wa medali angalau ya shaba lakini Weighman wa Australia akajikokota kutoka nyuma akidhamiria kuwakuta Wakenya lakini pengo lililojengwa mapema likawa kubwa kwa raia wa Australia kuziba akiridhika na shaba.

Ushindi wa Kenya katika mbio hizi za Marathon umeiweka Kenya juu ya Australia kwa wingi wa medali kutoka mashindano ya mbio kwa mara ya kwanza katika historia ya michezo ya Jumuia ya Madola.

Medali hii ni ya 11 katika mashindano ya mbio za kukimbia mjini Delhi mbali na medali zilizopatikana katika mashindano mengine kama kuogelea, ngumi au tennis.

Mashindano haya yanahitimishwa kwa tafrija ya maonyesho ya michezo yenye asili ya India kama vile mfumo wa kujikinga, Karate ambayo India inadai ni utamaduni ulioanzia hapa watawa wa Ki-Buddha walipokuwa wakieneza neno la kiongozi wao ilibidi wajifunze kutumia mfumo wa kujihami bila kutumia silaha.

Hivyo ndivyo Karate, Taekwondo na Jiu jitsu ilivyoanza kwa kuenezwa na watawa wa Kibuddha miaka mingi iliyopita.

Kenya yanyakua medali nyingi

Maonyesho yana muziki wa bendi ya jeshi la India kabla ya ushairi wa kusifu taifa la India kama 'Taifa Mama' wa mshairi na mtunzi AR Rahman.

Sherehe imehitimishwa kwa hotuba ya mwakilishi wa mashindano ya 20 huko Glasgow, Scotland mwaka 2012.

Baada ya hapo wanamuziki maarufu 29 kutoka kote duniani walishirikiana kuimba wimbo wenye shairi la penzi lisilo mipaka ya Kilimwengu.

Mbali na sherehe hizo, mashindano haya yameshuhudia wanariadha wawili wa Nigeria kupatikana kuwa walitumia dawa za kuongezea nguvu mwilini, na Rani Yadav wa India ambaye alishiriki mashindano ya kutembea na baada ya vipimo kupatikana kuwa naye alitumia dawa aina ya '19-Norandrosterone. Rani aliyeshiriki mashindano ya wanawake alimaliza wa sita.

Habari nyingine ni kwamba wanariadha wa India walioishindia medali za dhahabu wameahidiwa zawadi ya rupee milioni moja na serikali ya Delhi, mamlaka ya Reli imeahidi kutoa Rupee milioni moja na nusu halikadhalika serikali ya jimbo la Haryana milioni 1.5 sawa na dola 96,000.

Kwa upande wa mbio Kenya inamaliza ya sita kwenye msimamo wa medali, ikiwa na dhahabu 12 fedha 11 na shaba 9, ikilinganishwa na mshindano ya Jumuia ya Madola ya mwaka 2006 ilipovuna jumla ya medali 18.

Kenya imepiga hatua kubwa kwa kuongeza medali 14. Uganda iliyopata medali 3 mjini Melbourne safari hii imeondoka na mbili za dhahabu.

Tanzania iliyonyakua dhahabu wakati huo imepoteza taji lake la mbio za Marathon, Samson Ramadhan alipoishiwa na maarifa kwenye mashindano haya na kusalimu amri akionekana kurudi nyuma katika hatua za mwisho mwisho.

Pamoja na ulinzi mkali, viwanja vilivyojitenga na usafiri mgumu, joto kali na ukiritimba uliokithiri kwa kero Idhaa ya kiswahili imejitahidi kadri ya uwezo kukufikishia yote yaliyowahusu wana Afrika mashariki.