Mmiliki mpya anuia kuinyayua Liverpool

Mmiliki mpya wa Liverpool John W Henry ameahidi kupambana na matatizo yanayoikabili klabu hiyo nje na ndani ya uwanja.

Image caption John W Henry

NESV, kampuni inayoongozwa na Henry ilikamilisha umiliki wa Liverpool siku ya Ijumaa baada ya mvutano mkali wa kisheria katika mahakama za Uingereza na Marekani.

Henry amesema amefurahi na kujivunia hali hiyo kumalizika kwa usalama na akaongeza "nipo hapa kushinda": "Inatulazimu kufanya kazi kufa na kupona".

"Kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuifikisha klabu hii mahala inapostahili, lakini hapana shaka pamoja na vikwazo tutakavyokumbana navyo kazi hiyo tutaifanikisha."

Kampuni ya NESV hatimaye ilifanikiwa kushika hatamu za kuimiliki Liverpool kutoka kwa wamiliki wa awali Tom Hicks na taasisi ya Kimarekani ya fedha siku ya Ijumaa, kwa dau la paundi milioni 300, ambazo kwa kiasi kikubwa limepunguza madeni ya klabu hiyo.

Hicks ametishia kuchukua hatua za sheria kuhusiana na uuzwaji huo, ambapo amedai klabu hiyo imeuzwa kwa bei ya chini, lakini kwa sasa Henry anaagazia zaidi kuinyanyua Liverpool uwanjani na pia klabu hiyo kuwa na uwanja mpya au mradi mkubwa wa maendeleo hapo Anfield.

Henry ambaye pia anamiliki timu ya mchezo wa Baseball ya Marekani ya Boston Red Sox, amesema:"Kwa kweli katika kipindi cha miezi miwili kazi kubwa tuliyoifanya, imetudhihirishia changamoto na matatizo yaliyopo na hatuna budi kuyafanyia kazi".

Henry amesema kitendawili cha kujenga uwanja mpya ama kuukarabati uwanja wa sasa wa Anfield wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 45,000, ni sawa na kile kilichokuwa ikiikabili kampuni ya NESV ilipoinunua Red Sox na uwanja wake wa nyumbani wa Fenway Park mwaka 2002.

Liverpool kwa muda mrefu imekuwa na mipango ya kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 60,000 eneo la Stanley Park, karibu na uwanja wa sasa wa nyumbani wa Anfield lakini kazi hiyo haijaanza kutokana na matatizo ya fedha.