Man United hali ngumu, Arsenal yapeta

Timu ya Arsenal imefanikiwa kurejea nafasi ya pili iliyoiacha kwa muda mrefu katika Ligi Kuu ya Soka ya England, baada ya kuilaza Birmingham mabao 2-1. Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kufungwa kwa bao lililopachikwa na Zikola Zigic katika dakika ya 33. Dakika nane baadae Arsenal walisawazisha kwa mkwaju wa penalti uliopachikwa na Samir Nasir baada ya Marouane Chamakh kuangushwa na mlinda mlango wa Birmingham Ben Foster.

Image caption Samir Nasir

Marouane Chamakh aliipatia Arsenal bao muhimu la pili muda mfupi baada ya kuanza kipindi cha pili.

Katika pambano hilo mchezaji wa kutegemewa wa Arsenal Jack Wilshere alitolewa nje baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Zigic.

Kwa matokeo hayo Arsenal imerejea nafasi ya pili ikiwa na pointi 14.

Katika mchezo mwengine makosa ya mlinda mlango wa Manchester United Edwin Van Der Sar, yameigharimu timu hiyo pointi tatu muhimu na hatimaye kutoka sare ya mabao 2-2 na West Brom.

Manchester United ndio ilikuwa ya kwanza kufunga kwa bao la Hernandez dakika ya 5 ya kipindi cha kwanza baada ya kuuwahi mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja wa Nani. Bao la pili la Manchester liliwekwa wavuni dakika 20 baadae na mshambuliaji wa pembeni Nani.

Kipindi cha pili West Bromich walikianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza baada ya mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja kumgonga mlinzi wa Manchester United Patrice Evra na kuingia wavuni. Hiyo ilikuwa ni tano tu tangu kuanza kipindi cha pili na dakika tano baadae makosa ya mlinda mlango Van Der Sar kushindwa kudaka mpira wa juu hafifu yaliigharimu timu hiyo na kukosa pointi tatu baada ya Tchoyi kuuwahi mpira huo na kuujaza wavuni. Kwa matokeo hayo Manchester United wamebakia nafasi ya tatu wakiwa na pointi 14 na West Bromich wamesogea nafasi ya sita wakiwa na pointi 12.

Matokeo mengine wakicheza nyumbani Bolton, wamefanikiwa kuzoa pointi tatu baada ya kuilaza Stoke City mabao 2-1, matokeo yanayoipeleka Bolton hadi nafasi ya saba wakiwa na pointi 11.

Fulham wakiwa nyumbani walishindwa kufurukuta baada ya kulazwa mabao 2-1 na Tottenham, matokeo yanayoifanya Spurs nafasi ya tano wakiwa na pointi 14.

Wakicheza nyumbani New Castle baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Wigan, walifanikiwa kurejesha mabao hayo yote kipindi cha pili na kubakia nafasi ya 13 wakiwa na pointi 8. Wigan kwa matokeo hayo wanakamata nafasi ya 12 wakiwa na pointi 9.

Katika mchezo mwengine Wolves waligawana pointi na West Ham baada ya kwenda sare ya kufungana bao 1-1. Pamoja na matokeo hayo West Ham inaendelea kuburura mkia wakiwa na pointi 6, mbele ya Wolves nao wenye pointi 6.