Hodgson asema Torres hajiamini

Meneja wa Liverpool Roy Hodgson amekiri mshambuliaji wake Fernando Torres huenda ana matatizo ya kujiamini.

Image caption Fernando Torres

Torres amefunga bao moja tu msimu huu katika michezo 10 aliyocheza na hakufurukuta wakati Liverpool ilipolazwa mabao 2-0 na Everton siku ya Jumamosi.

Hodgson amesema:"Hana matatizo ya kuumia."

"Hakufanya vizuri wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia na nadhani kiakili mawazo yake hayako sawa. Anahitaji kufunga bao moja au mawili kurejesha kujiamini."

Torres alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya goti mwishoni mwa msimu uliopita na msimu huu ulipoanza akakumbwa na maumivu ya nyonga baada ya kuingizwa kipindi cha pili katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania na Uholanzi mwezi wa Julai nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo amekuwa katika kikosi cha kawaida cha Liverpool msimu huu na alicheza dhidi ya Everton, na katika mchezo dhidi ya Blackpool akatolewa kutokana na maumivu ya misuli.

Hodgson amesifu jitahada za mshambuliaji huyo katika mechi na Everton, ingawa kichwa alichopiga cha kinyumenyume dakika za mwisho mwisho hakikuweza kuipatia bao timu yake pamoja na kwamba kilikuwa cha hatari iliyosababisha kona.

Liverpool hadi sasa inashikilia nafasi isiyoizoea ya pili kutoka mkiani mwa Ligi Kuu ya England, wakiwa wameshinda mchezo mmoja kati ya minane waliyocheza.