Baada kukiri Gazza aonywa atafungwa

Mchezaji wa zamani wa soka wa England Paul Gascoigne, ameonywa anaweza kufungwa baada ya kukiri aliendesha gari akiwa amezidisha kiwango cha ulevi mara nne na inavyokubalika.

Image caption Paul Gascoigne

Gazza mwenye umri wa miaka 43 kiungo wa zamani wa England, alisomewa mashtaka yake katika mahakama ya Newcastle.

Gascoigne alisimamishwa na askari polisi huko Newcastle tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba.

Anatazamiwa kuhukumiwa mwezi ujao wa Novemba kwa kosa la kunywa pombe na kuendesha gari mwezi wa Februari huko North Yorkshire.

Siku ya Jumatano. Jaji wa mahakama ya wilaya Stephen Earl alimwambia Gascoigne alikuwa amekunywa miligram 142 za pombe wakati alipopimwa pumzi yake wakati aliposimamishwa huko Jesmond, Newcastle, tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba.

Kiwango kinachoruhusiwa cha kileo na kuendesha gari ni miligram 35.

Jaji Earl amesema uwezekano wa adhabu zote uko wazi, ikiwemo kifungo cha wiki 12 jela, kama sheria inavyosema kwa mtu anayendesha gari akiwa amekunywa pombe nyingi.

Jaji huyo alimpiga marufuku Gazza kuendesha gari hapo hapo.

Alisema atamhukumu Gascoigne tarehe 11 mwezi wa Novemba baada ya maandalizi ya ripoti ya kumwekwa chini ya uangalizi itakapokamilika.

Gascoigne anatarajiwa kukabiliana na hukumu nyingine ya makosa ya kuendesha gari akiwa amelewa tarehe 3 mwezi wa Novemba, katika mahakama ya Northallerton, North Yorkshire.

Enzi zake za usakataji kabumbu kwa miaka 20, Gascoigne alichezea klabu za Newcastle, Tottenham, Lazio, Rangers, Middlesbrough na Everton. Alichezea timu ya taifa ya England mechi 57.