Bingwa wa Olympic afungiwa miaka miwili

LaShawn Merritt
Image caption LaShawn Merritt

Bingwa wa Olympic na dunia wa mbio za mita 400 LaShawn Merritt amesimamishwa kushiriki mashindano yoyote kwa muda unaokaribia miaka miwili baada ya kugundulika ametumia dawa za kumuongezea nguvu.

Mkimbiaji huyo Mmarekani mwenye umri wa miaka 24 alipimwa na kukutwa ametumia dawa hiyo aina ya testosteronemara tatu kati ya mwezi Oktoba mwaka 2009 na mwezi Januari mwaka 2010.

Lakini kusimamishwa huko kwa kipindi cha miezi 21 kunaanzia tarehe 28 Oktoba mwaka 2009, ambayo ni siku ya kwanza aliyofanyiwa vipimo na kugundulika ametumia dawa hizo na kwa maana hiyo ataweza kushiriki mashindano ya ubingwa wa dunia ya mwezi Agosti mwaka 2011.

Merritt, ambaye alishinda mbio za mita 400 katika michezo ya Olympic iliyofanyika Beijing, alikubaliana na uamuazi huo.

"Mwanariadha huyo pia amepokonywa ushindi alioupa kuanzia tarehe 28 Oktoba mwaka 2009, zikiwemo medali, pointi na zawadi."

Mmarekani huyo ambaye pia alinyakua ubingwa wa dunia kwa mbio za mita 400 mashindano yaliyofanyika Berlin, amekiri kutumia dawa zinazomuongezea nguvu mwanaume.

Alidai mwezi wa April hakufahamu kuwa dawa alizotumia zilikuwa na chembechembe zilizopigwa marufuku na amekiri amefanya jambo la"kipumbavu, la kitoto na ni makosa makubwa".

Amesema katika taarifa aliyoitoa wakati huo: "Kufahamu nimegundulika kutumia kwa matumizi binafsi dawa zenye chembechembe zinazokatazwa kwa mwanariadha ni jambo gumu."

Merritt alishirikiana vizuri na maafisa wanaochukua vipimo vya wanamichezo, hali iliyomsaidia kupunguziwa kifungo kwa miezi mitatu.