Chelsea yaua, Arsenal yavunja rekodi

Fabregas na Chamakh wakipongezana
Image caption Fabregas na Chamakh wakipongezana

Arsenal imekaribia kucheza hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuivuruga Shakhtar Donetsk kwa mabao 5-1 na kushikilia usukani wa kundi H.

Mabao ya Arsenal yalipachikwa na Alexander Song, Samir Nasir, Cesc Fabregas, Jack Wilshere na Marouane Chamakh akahitimisha karamu ya mabao.

Bao pekee la kufutia machozi la Shaktar lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Eduardo.

Bao la Chamakh limemfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mechi sita mfululizo za Ubingwa wa Ulaya, lakini msisimko mkubwa ulikuwa kwa Eduardo, aliyecheza kwa mara ya kwanza uwanja wa Emirate tangu alipoihama timu hiyo na kujiunga na Shaktar kwa dau la paundi milioni 6.

Alipoingia katika dakika ya 63 uwanja mzima mashabiki walisimama na kumshangilia na hata alipofunga bao la kufutia machozi kwa Shaktar hata mashabiki wa Arsenal waliinuka na kushangilia bao lake.

Bao la Arsenal la tano ambalo limeifanya timu hiyo kufikisha mabao 14 hadi sasa katika mashindano ya mwaka huu, limeweka rekodi mpya ya Ubingwa wa Ulaya.

Nayo Chelsea imejihakikishia muelekeo mzuri wa kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya hatua ya mtoano, ikiwa ugenini kwenye baridi kali mjini Moscow, iliwalaza wenyeji wao Spartak kwa mabao 2-0.

Alikuwa Mrusi Yuri Zhirkov aliyeipatia Chelsea bao la kwanza kwa mkwaju wa mbali katika dakika ya 23.

Nicolas Anelka baadae akamalizia kazi dakika moja kabla ya mapumziko kwa kuandika bao la pili.

Kwa ushindi huo Chelsea wanaongoza kundi lao la F .

Matokeo mengine ya michezo ya Ubingwa wa Ulaya iliyochezwa siku ya Jumanne.

Ajax 2-1 Auxerre

Bayern Munich 3-2 CFR Cluj-Napoca

Image caption Fabregas na Chamakh wakipongezana

Braga2-0 Partizan Belgrade

Marseille 1-0 MSK Zilina

Real Madrid 2-0 AC Milan

Roma 1-3 Basle