Mateka aachiliwa huru Somalia

Image caption Makundi yenye silaha nchini Somalia huteka watu kila mara na kudai kikombozi

Mateka huyo Frans Barnard ameachiliwa mapema leo baada ya shinikizo kutoka kwa wazee wa kikoo na maafisa wa eneo hilo.

Bw.Barnard, mzaliwa wa Zimbabwe, amekuwa akifanya kazi kama mshauri wa masuala ya usalama katika shirika la misaada la Uingereza la Save the Children katika mji wa Adado karibu na mpaka wa Ethiopia.

Alitekwa nyara alhamisi wiki iliyopita nje ya hoteli alipokuwa akiishi. Mkuu wa eneo hilo, Mohammed Aden, alisafiri hadi nje ya mji huo ambako jamaa huyo alikuwa anashikiliwa mateka na kufanya mashauriano na kundi lilomteka.

Bw. Aden anaaminiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya mashuriano na makundi kama haya.

Haijathibitishwa iwapo kikombozi chochote kilitolewa ili mateka huyo aachiliwe huru.

Shirika la Save the Children limethibitisha kuwa Bw. Barnard yuko safarini akielekea eneo lenye usalama na limekanusha madai kwamba kikombozi kilitolewa.

Makundi yaliojihami huwateka nyara mara kwa mara wafanya kazi wa mashirika ya kutoa misaada nchini Somali na kisha kudai kikombozi.