Chelsea yazidi kujichimbia kileleni

Vinara wa ligi kuu ya soka ya England Chelsea, wamezidi kutanua wigo wa ponti hadi tano baada ya kuilaza Wolves waliopigana kiume mabao 2-0.

Image caption Chelsea wajichimbia kileleni

Wolves walijitahidi kutafuta nafasi kadha katika mchezo uliokuwa wazi huku David Edwards na Kevin Doyle wakilikaribia mara kwa mara lango la wapinzani wao.

Lakini uwezo mkubwa wa ushambuliaji wa Chelsea uliwasaidia na alikuwa Florent Malouda aliyepachika wavuni bao la kwanza baada ya pasi ya Yuri Zhirkov.

Mabingwa hao watetezi walipoteza nafasi nyingi za wazi kabla ya Salomon Kalou aliyeingia kipindi cha pili kupachika bao safi la pili.

Kwa ushindi huo Chelsea wanazidi kujishindilia kileleni mwa masimamo wa ligi kuu ya soka ya England wakiwa na pointi 22.

Katika mchezo mwengine West Brom imeweza kujisogeza katika timu nne bora za juu, baada ya kuwalaza Fulham mabo 2-1 na kufikisha pointi 15 na kushikilia nafasi ya nne.

Fulham inaendelea kuwa timu ambayo haijapata ushindi wa ugenini.

Sunderland nayo imejisogeza nafasi ya saba baada ya kuwalaza Aston Villa 1-0. Birmingham wakicheza nyumbani wameweza kuutumia vyema uwanja wao kwa kuwalaza Blackpool mabao 2-0. Kwa ushindi huo Birmingham wameweza kusogea hadi nafasi ya 11.

Wigan waligawana pointi na Bolton baada ya kufungana bao 1-1.

Katika mchezo wa mapema Tottenham walishindwa kuutumia uwanja wao wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na wagumu wa Everton. Hata hivyo Tottenham wameweza kujinyanyua hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 15.