Vuvuzela kupigwa marufuku Afrika Kusini

Vuvuzela huenda zikapigwa marufuku katika viwanja vya soka nchini Afrika Kusini kama mashabiki klabu ya Kaizer Chiefs hawataacha vurugu zao.

Image caption Mshabiki wa soka akipuliza vuvuzela

Katika mechi za hivi karibuni, mashabiki wa klabu hiyo maarufu sana nchini humo, walirusha uwanjani vuvuzela mbili pamoja na kabichi.

Klabu huyo ya Kaizer Chiefs imefungiwa na kupigwa faini ya dola 72,130, huku mwenyekiti wao ameamriwa kuomba radhi hadharani.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Ligi Kuu ya soka ya Afrika Kusini, Zola Majavu, "iwapo vuvuzela zitaendelea kutumika kama silaha, huenda zikapigwa marufuku.

Mashabiki wengi wa soka walioangalia fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini kupitia televisheni zao, walikuwa wakiomba vuvuzela zipigwe marufuku.

Hata hivyo, maelfu ya mashabiki wa soka walikuwa wakienda viwanjani na vuvuzela zao, huku mashabiki kutoka nje ya nchi walinunua bidhaa hiyo ikiwa ni ishara ya kombe la dunia kufanyika Afrika Kusini mwaka 2010.

Klabu hiyo ya Chiefs pia iliamriwa kulipa dola 3,000 gharama za kusikiliza shauri la nidhamu na wameambiwa waitishe mkutano wa waandishi wa habari kushutumu utovu wa nidhamu uliooneshwa na mashabiki wao.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Kaizer Motaung amewataka mashabiki wao kutoa msaada wa kuwatambua wale wanaofanya fujo.

"Mara tutakapowatambua itatuwia rahisi kuwabana na kuwapiga marufuku viwanjani."

Katika miaka ya karibuni, mashabiki wa soka nchini Afrika Kusini, wameanza tabia ya kwenda na mikate pamoja na kabichi uwanjani, wakila mbele ya kamera za televisheni wakiashiria wanawatafuna wapinzani wao.