Usain Bolt apona na yu tayari kushindana

Usain Bolt amesema amepona kabisa majeraha yaliyomfanya asikimbie kwa miezi kadha.

Image caption Gay alipomshinda Bolt

Mkimbiaji huyo wa mbio fupi mwenye kasi kuliko binadamu yeyote kwa wakati huu, aliamua kupumzika kuganga majeraha yake tarehe 10 mwezi Agosti, siku nne baada ya kushindwa na Tyson Gay katika mbio za mita 100 zilizofanyika Stockholm.

Lakini bingwa huyo wa michezo mitatu wa Olympic mwenye umri wa miaka 24, ameanza mazoezi na anakusudia kutetea mataji yake ya ubingwa wa dunia ya mbio za mita 100 na 200 katika mashindano yatakayofanyika Korea mwaka 2011.

Bolt amesema: "Habari nzuri ni kwamba sasa amepona kwa silimia 100 na matatizo ya mgongo na kisigoni yaliyokuwa yakimsumbua yamekwisha."

Bolt hakuweza kumalizia mashindano ya ligi ya kuwania almasi yaliyofanyika Zurich na Brussels baada ya kushindwa na Gay kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka miwili nchini Sweden.

Mkimbiaji huyo Mjamaica halikadhalika hakuweza kushiriki mashindano ya Jumuia ya Madola ya India mwezi wa Septemba, wakati huo akiwa bado anasumbuliwa na maumivu ya mgongo.

Lakini Bolt, aliyeweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za mita 100 katika mashindano ya ubingwa wa dunia ya Berlin mwezi Agosti mwaka 2009, ameeleza sasa yupo tayari kurejea uwanjani kwa kishindo.