Bongani Khumalo kujiunga na Tottenham

Klabu ya Tottenham imefikia makubaliano ya awali kumsajili mlinzi wa Afrika Kusini Bongani Khumalo kufuatia kufanya vizuri katika majaribio.

Image caption Bongani Khumalo kujiunga na Spurs

Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 23 aliyecheza katika mashindano ya Kombe la Dunia na awali alihusishwa kujiunga na klabu ya Rangers ya Scotland, atajiunga na Spurs akitokea klabu ya SuperSport United itakapofika mwezi wa Januari kwa dau la paundi za Uingereza milioni 1.5.

Hata hivyo yote hayo yatategemea upatikanaji wa kibali cha kufanya kazi.

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp alisema mwezi wa Septemba: "Mchezaji huyo si ghali. Tumekuwa naye kwa majaribio na tumempenda."

Khumalo aliyezaliwa Swaziland, aliichezea Afrika Kusini katika mechi zote tatu za Kombe la Dunia na alifunga bao wakati Bafana Bafana walipoilaza Ufaransa kwa mabao 2-1.

Kuwasili kwa mlinzi huyo itakuwa afueni kubwa kwa safu ya ulinzi ya Tottenham, wakati huu walinzi wao wa kutegemewa Michael Dawson na Jonathan Woodgate wakiwa majeruhi.

Khumalo atajiunga na Tottenham wakati wa msimu wa usajili mdogo utakapofunguliwa tarehe 1 mwezi wa Januari na akizungumza baada ya mashindano ya Kombe la Dunia, alisema itakuwa "ndoto" kwake kuweza kucheza katika Ligi Kuu ya England.