England kuisamehe Urusi

Kamati ya inayoandaa mchakato wa England kuwa wenyeji wa kombe la dunia 2018 imepanga kuondoa malalamishi dhidi ya Urusi kwa FIFA kufwatia Urusi kuomba radhi.

Urusi pia inawania kuwa wenyeji wa kombe hilo mwaka 2018.

Waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko ameomba radhi kwa matamshi ya Alexei Sorokin,ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kamati ya Urusi.

Malalamishi rasmi ya England ni kwamba Urusi imekiuka kanuni za kuomba kuwa wenyeji wa kombe la dunia kwa kutoa matamshi mabaya juu ya jiji la London.

Kamati ya FIFA ilikutana siku ya Alhamisi kupokea ripoti kwa nchi zenye nia ya kuwa wenyeji wa kombe hilo.

Kamati ya England ililalamika siku ya Jumanne, kwamba Sorokin alizungumzia "kiwango kikubwa cha uhalifu" jijini London na matatizo ya vijana kunywa pombe.

Alisema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari wa Urusi jambo ambalo linaonekana kukiuka sheria za FIFA za kutozungumzia wapinzani wako.