Fifa yaifungulia Nigeria rasmi

Fifa imeiondoa rasmi marufuku iliyoiwekea Nigeria baada ya kesi mahakamani dhidi ya maafisa wa Shirikisho la Soka kufutwa.

Image caption Fifa yaifungulia Nigeria

Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) lilifungiwa wiki tatu zilizopita kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kuingiliwa kisiasa na serikali.

Marufuku hiyo awali iliondolewa siku chache baadae ambapo Nigeria iliruhusiwa kucheza mechi ya kufuzu mashindano ya kuania Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Guinea.

Kuondolewa kwa hatua za kisheria na chama cha wachezaji (NANF) imetoa ruhusa kwa NFF kuendesha shughuli zake upya, hali iliyoifanya Fifa kufuta adhabu ya kuifungia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Fifa iliyotolewa siku ya Ijumaa: "Fifa imeamua kuondoa adhabu ya kulisimamisha Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) baada ya kupokea uthibitisho kwamba hatua za kuwapeleka mahakamani wajumbe wa NFF imesimamishwa na kwa sasa wanaweza kufanya kazi bila pingamizi lolote.

Fifa awali iliifungia Nigeria kwa kile ilichoita "serikali kuingilia kati" uendeshaji wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo baada ya kutolewa mapema katika fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Lakini ilisimamisha hatua hiyo mapema mwezi wa Oktoba, hadi tarehe 26 baada ya baadhi ya hatua kuchukuliwa, na kutoa ruhusa ya nchi hiyo kucheza mechi dhidi ya Guinea ya kufuzu mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012.

Kaimu Katibu Mkuu wa NFF Musa Amadu alisema, kuondolewa wiki hii kwa kikwazo cha mwisho, kesi mahakamani ya Chama cha soka cha Taifa nchini Nigeria (NANF), kimetoa ruhusa kwa Shirikisho la soka kufanya kazi zake upya.