Shughuli ya kupiga kura inaendelea Tanzania

Raia wa Tanzania wanaendelea na shughuli ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu.

Image caption Wafuasi wa chama cha CCM

Kuna ushindani mkali katika kinyanganyiro cha kuwania kiti cha urais.

Miongoni mwa watu wanaowania kiti hicho ni pamoja na rais wa sasa Jakaya Kikwete, ambaye alizoa asilimia 85 ya kura zote zilizopigwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Wakosoaji wa Rais Kikwete wanasema ameshindwa kukabiliana na ufisadi na kuhakikisha kuwa rasilimali ya nchi inawafikia raia wa kawaida.

Image caption Wilbrod Slaa

Rais Kikwete anapambana na wapinzani wengine akiwemo Willibrod Slaa, ambaye ameahaidi kupambana na ufisadi na kuanzisha huduma za afya na elimu bila malipo nchini humo endapo atachaguliwa kuongoza taifa hilo.

Mwingine ni Ibrahim Lipumba ambaye amehaidi kubuni serikali ya muungano wa kitaifa ili kutatua matatizo ya taifa ikiwa atashinda uchaguzi huo.

Wapiga kura milioni 19.6 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.

Mwandishi wa BBC Kisiwani Zanzibar anasema matatizo kadhaa yameanza kujitokeza katika majimbo kadhaa.

Anasema kura za kuwachagua wabunge hazikutokea na hivyo kuwalazimisha kukosa kuwachagua wabunge wao.

Licha ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha kisiwani Pemba idadi kubwa ya wapiga kura wanaendelea kujitokeza.