Blackpool yailaza 2-1 West Brom

Blackpool ilitumia vizuri kutolewa katika kipindi cha kwanza kwa kuoneshwa kadi nyekundu wachezaji wawili wa West Brom na kuweka rekodi ya kushinda katika uwanja wao wa nyumbani tangu mwaka 1971 katika mchezo wa Ligi Kuu ya England.

West Brom walipata pigo lao lao la kwanza mapema tu dakika ya 10 kipindi cha kwanza baada ya mlinzi wao Pablo Ibanez alipotolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha ndani ya sanduku la hatari mshambuliaji wa Blackpool DJ Campbell, hali iliyosababisha itolewe penalti ambayo iliwekwa kimiani na Charlie Adam.

Rafu mbaya na isiyokuwa na sababu yoyote iliyofanywa na mlinzi mwengine wa West Brom Gonzalo Jara dhidi ya Luke Varney iliwaweka pabaya Baggies na kucheza wakiwa wachezaji tisa.

Alikuwa Varney aliyeipatia bao la pili na la ushindi Blackpool katika dakika ya 62, kabla ya kiungo wa West Brom Mulumbu kufunga bao la kufutia machozi.

Kwa matokeo hayo Blackpool wamesogea hadi nafasi ya tisa wakikusanya pointi 13.