Mwenyekiti wa haki na maridhiano nchini Kenya ajiondoa

Machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2007 nchini Kenya
Image caption Machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2007 nchini Kenya

Mwenyekiti wa tume ya haki,ukweli na maridhiano nchini Kenya ameamua kujiondoa ili kutoa nafasi wa jopo maalum kufanya uchunguzi kwa madai dhidi yake.

Katika kujiondoa kwake Balozi Kiplagat hakujitokeza moja kwa moja kuwahutubia waandishi wa habari bali alituma taarifa kwa vyombo vya habari.Kwenye taarifa hiyo alisema kuwa anaamini haki ya kimsingi ya kila mkenya kutokuwa na hatia hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi kuwa mtu ana hatia.

Katika siku za awali Kiplagat alikataa kuondoka kwenye wadhifa wa menyekiti licha ya wito wa yeye kuondoka ili kutoa nafasi kwa tume hiyo kufnya kazi yake bila pingamizi.

Muda wote huo alisisitiza kwamba angependa jopo la kisheria kuundwa ili kumchunguza.

Wiki iliopita,kamti ya haki na masuala ya sheria ya bunge iliwapa tume hiyo saa 72 kuweka mambo yake sawa au bunge lianze mchakato wa kuvunja kamati hiyo.

Baadhi ya makamishna wamefurahishwa na hatua hiyo ya kujiondoa kwa Kiplagat.

''Tumefurahi sana kwa sababu raia wa Kenya watapata haki yao na sisi wenyewe tumeridhika,sasa tutapata pesa kutoka kwa serikali na wafadhili na tuftafanya kazi yetu vizuri,'' alisema kamishna Ahmed Farah.

Jukumu la tume ya haki,ukweli na maridhiano ilikuwa kufanya uchunguzi juu ya ukiukwaji wa haki za binaadamu ikiwemo yale yaliofanywa na serikali na makundi mengine.Masuala ni machafuko yaliyochochewa siasa,mauaji na watu kuachwa bila makaazi.