Watu 3 watuhumiwa kufadhili Alshabab

Wapiganaji wa alshabab Somalia
Image caption Wapiganaji wa alshabab Somalia

Wanaume watatu katika jimbo la California nchini Marekani wameshtakiwa kwa kulisaidia kundi la kigaidi la kiislam la al-Shabab, la nchini Somalia.

Kwa mujibu wa wizara ya masuala ya haki ya Marekani, watu hao wakazi wa mji wa San Diego wamekuwa wakifadhili harakati za kundi hilo kwa kutoa misaada ya fedha na kuunga mkono shughuli nyingine za kundi hilo. Washukiwa hao - Basaaly Saeed Moalin, Mohamed Mohamed Mohamud na Issa Doreh - walikamatwa Jumapili na Jumatano.

Wanakabiliwa na mashtaka ya kuwasambazia wapiganaji wa Al Shabab vifaa vya kutumia vitani, kufadhili kundi la kigeni la kigaidi na njama ya kutekeleza mauaji katika taifa la kigeni miongoni mwa mashtaka mengine.

Inadaiwa washukiwa hao walishirikiana na aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa al-Shabab Moalim Aden Hashi Ayro, aliyeuawa katika mashambulizi ya ndege za kivita za Marekani yaliyotekelezwa mwaka 2008.

Moalin anasemekana alikuwa akifanya juhudi za kuchangisha fedha na kuzifikisha kwa kundi hilo la Al Shabab kufuatia amri ya Ayro. Na aliendelea kufanya hivyo hata baada ya kifo cha Ayro.

Maombi ya Moalin kuachiliwa kwa dhamana yamekataliwa na atasalia gerezani. Kesi dhidi yake itasikilizwa tena Ijumaa.

Kundi la Al shabab limedai kuwa lilitekeleza mashambulizi ya mabomu yaliyotokea mjini Kampala,Uganda yaliyowauwa watu 76 mwezi Julai. Wanajeshi wengi wa muungano wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia ni raia wa Uganda.

Kundi hilo linadhibiti mengi ya maeneo ya kusini nchini Somalia. Tangu mwaka 1991 nchi hii haijawa na serikali thabiti.