Wachezaji wa Ghana hawajalipwa bonasi

Mafanikio ya kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia yamezua mzozo unaohusu malipo ya ziada waliyoahidiwa wachezaji wa timu ya taifa ya Ghana.

Image caption Wachezaji wa Ghana

Hakuna mchezaji hata mmoja aliyelipwa dola 63,000 alizoahidiwa kila mchezaji wa Black Stars kwa sababu taratibu za malipo katika benki ya Ghana.

Benki Kuu ya Ghana inasisitiza kuwalipa wachezaji hao kwa kuwawekea pesa katika akaunti zao.

Lakini wachezaji wamekuja juu kwa vile wanataka walipwe fedha taslimu mkononi kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Taarifa ya Benki Kuu ya Ghana imesema benki hiyo hufanya kazi zake za kuwahudumia wateja kwa taratibu zilizopo na kutofanya hivyo ni kwenda kinyume na shughuli za uendeshaji benki ambapo wakiwalipa fedha taslimu zinaweza kuzidi kwa zaidi ya dola 10,000.

Benki Kuu ya Ghana imeiambia Wizara ya Vijana na Michezo watawalipa wachezaji wa Black Stars kwa fedha za kigeni kupitia akaunti zao au kwa hundi.

Mzozo huo wa malipo ya wachezaji uligubika pambano la kufuzu katika michezo ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Sudan.

Tarehe ya mwisho ya kulipwa wachezaji hao ilikuwa 15 mwezi wa Oktoba na hakuna senti hata moja waliyolipwa wachezaji hao.