Jisung Park aiponya Man- U

Park Ji-Sung alifunga mabao mawili, moja katika muda wa ziada na kuipatia Manchester United ushindi wa 2-1 dhidi ya Wolverhampton katika uwanja wa Old Trafford.

Image caption Park Ji- Sung

Hali iliashiria mchezo ulikuwa unakwenda kumalizika kwa sare ya moja kwa moja, kufuatia bao la kusawazisha la Wolverhampton lililofungwa na Sylvan Ebanks-Blake katika dakika ya 66.

Park alikuwa ameifungia Manchester United bao la kwanza, sekunde chache kabla ya muda wa mapumziko.

Umiliki wa mpira ulikuwa 50-50, huku Kevin Doyle akiisumbua sana ngome ya Manchester United.

Kwa matokeo hayo Man U sasa wamefikisha pointi 23 na wamo katika nafasi ya pili, nyuma ya Chelsea, vinara wa ligi hiyo.

Awali Tottenham walizabwa mabao 4-2 na Bolton, matokeo yaliyozua maswali juu ya uwezo wao katika ligi ya mabingwa wa ulaya, na ligi ya nyumbani inawasumbua.

Ni hivi karibuni tu ambapo Spurs waliwafunga Inter-milan mabao 3-1 kwenye mchuano wa ligi ya mabingwa wa ulaya, huku Gareth Bale akitamba, lakini jumamosi alikuwa kivuli tu.

Bolton sasa imepanda hadi nafasi ya tano.

Mshambuliaji wa Ghana Asamoah Gyan alifunga mabao mawili na kuiwezesha Sunderland kuishinda Stoke mabao 2-0.

Ushindi huo umeiwezesha Sunderland kusogea hadi nafasi ya saba.

Kwenye matokeo mengine Fulham ilitoka sare 1-1 na Aston Villa nayo West Ham ikapata sare ya ugenini ya 2-2 dhidi ya Birmingham.

Sare nyingine ilikuwa ya Blackpool dhidi ya Everton waliofungana mabao 2-2.

Blackburn Rovers waliutumia vyema uwanja wa nyumbani walipowafunga Wigan 2-1.