Haile Gebreselassie astaafu riadha

Mwanariadha wa mbio ndefu za marathon anayeshikilia rekodi ya dunia Haile Gebrselassie ametangaza kustaafu riadha.

Image caption Haile Gebreselassie

Gebrselassie raia wa Ethiopia ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 37, alitangaza kustaafu baada ya kujitoa kwa mara ya kwanza katika mashindano ya marathon ya New York, baada ya kukimbia maili 16 akiwa anasumbuliwa na maumivu ya goti.

Bingwa huyo mara mbili wa michezo ya Olympic alisema: "Sikuwa nafikiria suala la kustaafu. Lakini kwa mara ya kwanza, siku imefika".

Gebrselassie aliweka rekodi ya dunia ya mbio za marathon ya saa mbili, dakika tatu na sekunde 59 mjini Berlin mwaka 2008.

Ilikuwa ni moja ya rekodi zake 27 bora alizoweka duniani katika kipindi chake cha mchezo wa riadha, ambapo aliweza kujizolea mataji manane ya dunia tangu mwaka 1993, kuanzia mbio za mita 1,500 hadi mbio za marathon.

"Wacha nifanye kazi nyingine," aliongeza. "Naona niwaachie vijana. Nimefanya kazi kubwa kushinda mbio hizi, lakini haikuzaa matunda."

Gebrselassie, mara ya kwanza kuchomoza katika ulimwengu wa riadha na kujulikana ni pale aliposhinda mbio za ubingwa wa dunia za mita 10,000 alipopata medali ya dhahabu akiwa na umri wa miaka 20 mjini Stuttgart, Ujerumani mwaka 1993, alistaafu kukimbia mbio za ndani ya viwanja na kuamua kujitosa katika mbio ndefu za marathon baada ya kumaliza nafasi ya tano mwaka 2004 wakati wa fainali ya mashindano ya Olympic ya Athen.

Alishinda medali ya dhahabu mjini Atlanta mwaka 1996 na Sydney miaka minne baadae.

Bingwa huyo wa dunia aliyeshiriki mashindano makubwa ya riadha mara 130, alifanyiwa uchunguzi wa goti lake kabla ya mbio za Jumapili za New York, ambapo goti lake lilionekana lina maji na limevimba, alijipanga kwa mbio hizo na hakuweza kumaliza.