Ruto arejea Kenya kutoka The Hague

Wiliam Ruto na wanasiasa Charle Keter na Joshua Kutuny
Image caption Wiliam Ruto na wanasiasa Charle Keter na Joshua Kutuny

Mwanasiasa mashuhuri nchini Kenya, William Ruto, ambaye alifanya ziara mjini The Hague Uholanzi kukutana na waendesha mashataka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) amerejea nchini Kenya.

Bw Ruto amesema ana furaha alipata fursa ya kuzungumza na wachunguzi wa mahakama hiyo na pia maafisa katika afisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, Luis Moreno Ocampo.

Waziri huyo wa zamani wa Elimu ya Juu nchini Kenya, aidha amekanusha madai ya baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya kwamba lengo la ziara yake lilikuwa kuwahusisha watu zaidi katika uchunguzi wa machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Ruto amesema,''Mimi sikwenda kufanya mkutano huo kwa nia ya kumshtaki mtu yeyote, ama chama chochote, au kiongozi yeyote''.

William Ruto alikwenda The Hague, Jumatano iliyopita kuelezea kile anachofahama kuhusu mapigano baada ya uchaguzi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1200 na wengine wapatao 250,000 kuachwa bila makazi.

Mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita inachunguza mapigano ya baada ya uchaguzi mwaka 2007.

Bw Ruto amekanusha kuhusika katika machafuko hayo, japo shirika la kutetea haki za binadamu, linalofadhiliwa na serikali limemtuhumu kuhusika.