Obama ahimiza wanasiasa wavumiliane Iraq

Viongozi wa Iraq
Image caption Waziri Mkuu Nouri al Maliki anatarajiwa kuunda serikali ya muugano baada ya mwezi mmoja

Rais Barack Obama wa Marekani amewataka viongozi nchini Iraq wavumiliane na wauunde serikali ambayo itashirikisha kila kundi la kisiasa nchini humo.

Katika taarifa kutoka ikulu ya White House, Rais Obama amesisitiza kuwa kila kundi lazima liwakilishwe kwenye ngazi za utawala nchini humo.

Kauli ya kiongozi huyo wa Marekani imetolewa baada ya mzozo ulioibuka bungeni pale Waziri Mkuu Nouri al Maliki, alipoombwa aunde serikali mpya na Rais Jalal Talabani.

Mpinzani wake na kiongozi wa kundi la Wasunni, Iyad Allawi alipinga hatua hiyo na kuongoza kundi lake kutoka bungeni.

Juhudi za kuunda serikali mpya nchini Iraq zimekwama, miezi nane baada ya uchaguzi.

Waziri Mkuu Maliki sasa ana kipindi cha mwezi mmoja ambapo anatarajiwa kumshawishi Bw Allawi ajiunge na serikali yake.