Nigeria kuihoji Iran kuhusu silaha

Nigeria
Image caption Silaha zilizokamatwa

Iran imeruhusu Nigeria kumhoji raia wa Iran aliyepo kwenye ubalozi wa Iran nchini Nigeria, kuhusiana na kukamatwa na shehena ya silaha mjini Lagos.

Iran ilituhumiwa kuhusika na silaha hizo na kulikuwa na taarifa kuwa Nigeria ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitishia silaha hizo kupelekwa sehemu nyingine.

Lakini taarifa za kuisalama zinasema Iran imeahidi kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo.

Kuishitaki UN

Nigeria imesema itaishitaki Iran kwenye Umoja wa Mataifa iwapo uchunguzi utaonesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa vimekiukwa.

Iran imewekewa vikwazo kutokana na mipango yake ya nyuklia.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Manoucher Mottaki amekwenda nchini Nigeria kujadili suala hilo na waziri wa mambo ya nje wa Nigeria Odein Ajumogobia, ambaye ameiambia BBC kuwa nchi hizo mbili zingependa kumaliza suala hilo.

Ushirikiano

Bw Ajumogobia amesema Bw Mottaki ameahidi kutoa ushirikiano katika uchunguzi, na ametoa idhini kwa mamlaka za Nigeria kuzungumza na mshukiwa aliyepo ndani ya ubalozi wa Iran nchini Nigeria.

Nigeria pia inataka kumhoji raia mwingine wa Iran aliyepo ndani ya ubalozi, lakini hatua hiyo imeshindikana kwa kuwa mtu huyo ana kinga ya kibalozi.