Suu Kyi aachiliwa huru

Serikali ya kijeshi nchini Burma imemuachilia huru kiongozi mwanaharakati wa demokrasia Aung San Suu Kyi.

Image caption Aung San Suu Kyi

Bi Suu Kyi amejitokeza mbele ya umati wa wafuasi wake waliokwenda nyumbani kwake mjini Rangoon, ambapo vizuizi vilivyowekwa karibu na nyumba yake vimeondolewa na mafisa wa usalama.

Mshindi huyo wa Nobel alikuwa amewekwa kizuizini kwa miaka 15 katika kipindi cha miaka 21 iliyopita.

Masharti

Mapema, mwanasheria wa Bi Suu Kyi alionya huenda asingekubali masharti ya kuachiliwa huru, iwapo yangemkataza kushiriki siasa.

Serikali ilimuwekea vikwazo vya kusafiri na kushiriki siasa wakati ilipokuwa ikumuachia huru katika vipindi vifupi siku za nyuma, na pia kumtaka aache siasa.

Awali alitakiwa kuachiliwa huru, kutoka kufungo cha nyumbani mwaka jana, lakini kesi inayomhusu Mmarekani aliyeogelea katika ziwa Inya kuelekea nyumbani kwake akidai kwenda kumuokoa, ilisababisha kifungo cha hivi karibuni.

Jumapili iliyopita, chama cha kisiasa kinachoungwa mkono na serikali ya kijeshi kilipata ushindi katika uchaguzi wa kwanza katika kipindi cha miaka 20. Uchaguzi huo ulishutumiwa vikali.