Kuumia kwa Torres kwaifungisha Liverpool

Bosi wa Liverpool Roy Hodgson anadhani kuumia kwa Fernando Torres kumechangia timu yake kufungwa mabao 2-0 na Stoke, lakini ameonesha matumaini tatizo la Torres si kubwa sana.

Image caption Roy Hodgson

Liverpool walikuwa wakihaha kutokana na bao la kwanza la Ricardo Fuller baada ya Torres kuchezewa rafu na waliruhusu bao la pili lililopachikwa na Kenwyne Jones kwa urahisi.

Hodgson amesema: "Tulimkosa Fernando Torres katika kipindi cha pili, aligongwa mguuni na ameumia kisigino."

"Lakini tunayo wiki nzima kabla ya mchezo unaofuata na yapo matumaini mambo yatakuwa safi." Alisema Hodgson.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa muda wa miaka 26 Stoke kuifunga Liverpool katika pambano la ligi na Hodgson anadhani wachezaji wake walishindwa kukabiliana na nguvu ya wapinzani wao na mbinu walizotumia za soka.

Hodgson amesema:"Stoke ni timu ngumu kuifunga kwao. Walikuwa na nguvu kutushinda. Walitubana na kutumia makosa yetu na hawakutupa nafasi ya kumiliki mpira, lakini hilo ndio tulilotazamia.

"Fernando hakutaka kutoka na sikutaka kumtoa, lakini hakuwa katika hali yake ya kawaida ya kufyatua mikwaju.

Meneja wa Stoke Tony Pulis, ambaye timu yake imesogea kutoka eneo la hatari la kushuka daraja hadi nafasi ya kumi, juu ya Liverpool kwa nafasi moja kwa idadi ya wingi wa mabao, amesema mbinu zao zilifanikiwa.