Pacquiao amtandika Margarito kwa pointi

Manny Pacquiao amezidi kujidhihirisha ni bondia bora duniani baada ya kutawala pambano lake na Antonio Margarito na kufanikiwa kutetea taji lake la dunia uzani wa kati linalotambuliwa na WBC.

Image caption Manny Pacquiao

Mfilipino huyo mwenye umri wa miaka 31 alishinda kila raundi ya pambano hilo kwa pointi nyingi, wakati mpinzani wake raia wa Mexico, alimaliza mpambano huo akitiririkwa na damu, pambano lililofanyika Dallas.

Pacquiao, ambaye pia ni mbunge nchini kwake, mara kwa mara katika raundi ya 11 alikuwa akimsihi mwamuzi Laurence Cole kusimamisha pambano.

Lakini hata hivyo pambano hilo liliendelea na Pacquiao akashinda taji la nane.

Jaji mmoja alitoa pointi 120-109, wakati wengine wawili walitoa pointi 119-109 na 118-110.

Pacquiao, ambaye alipanda uzito, bado kwa mara nyingine alishindwa kuudhibiti sawasawa uzani wa kati wa Margarito, alisema: "Siamini kwamba nimempiga mtu mwenye mwili mkubwa namna hii na mwenye nguvu.

"Nilimwambia mwamuzi, 'Angalia macho yake, angalia jinsi alivyochanika'. Nisingependa kumletea ulemavu wa kudumu. Mchezo wa ngumi hautaki hivyo."

Takwimu za ngumi zilizorushwa ulingoni zilionesha Pacquiao alirusha ngumi nyingi, akifanikiwa kuporomosha ngumi 474 dhidi ya 229 za Margarito. Lakini haikuwa tu wingi wa mvua za ngumi zilizorushwa, lakini ni ile nguvu ya ngumi zilizokuwa zikivurumishwa kutoka kila upande.

Na licha ya kutawala pambano hilo, Pacquiao alibainisha aliumizwa na Margarito katika raundi za katikati, baada ya kupigwa ngumi kichwani na mwilini.

Hata hivyo, Pacquiao alimudu kuvurumisha makombora ya masumbwi kama ilivyo kawaida yake.

"Manny ni bondia bora duniani," alisema mwalimu wa Margarito, Robert Garcia. "Ana kasi ya ajabu, anarusha ngumi haraka sana."