Defoe aanza mazoezi na Tottenham

Mshambuliaji wa Tottenham Hotspur Jermain Defoe ameanza mazoezi ikiwa ni karibu mwezi mmoja kabla ya wakati aliotarajiwa kurejea uwanjani.

Image caption Jemaine Defoe

Defoe mwenye umri wa miaka 28 alifanyiwa upasuaji wa kisigino baada ya kuumia wakati akiichezea England dhidi ya Switzerland tarehe 7 mwezi wa Septemba, katika mchezo wa kufuzu kwa mashindano ya Euro 2012.

Alitarajiwa kutocheza soka kwa miezi mitatu, lakini siku ya Jumanne mshambuliaji huyo alifanya mazoezi na wenzake wa Spurs ambao hawako katika timu zao za taifa.

Msimu uliopita Defoe alikuwa mfungaji bora, ambapo aliweka kimiani mabao 24 katika mashindano yote timu hiyo iliyocheza.

Kurejea haraka kwa Defoe pia kumemrudishia matumaini kocha wa England Fabio Capello.

Siku ya Jumatatu Spurs walithibitisha kiungo wao Tom Huddlestone atafanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya kisigino yanayomsumbua, hali itakayomfanya asicheze soka kwa miezi mitatu.