DRC yajitoa kuwaniai Ubingwa Afrika 2015

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetangaza kujitoa katika kinyag'anyiro cha kuandaa mashindano ya ubingwa wa soka kwa mataifa ya Afrika mwaka 2015 au 2017.

Image caption Bendera ya DRC

Rais wa Shirikisho la soka la Congo Omari Selemani, ameiambia BBC, matatizo ya uchumi na miundombinu yamewafanya kujitoa katika mbio hizo.

Selemani amesema: "Serikali inakabiliwa na majukumu mengi kwa miaka michache ijayo."

Ameongeza serikali haiwezi kuwa na vitegauchumi vinavyohitajika kwa ajili ya mashindano hayo.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) kupitia mtandao wake imesema: "Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, imewaarifu juu ya kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwania kuandaa mashindano hayo."

Morocco na Afrika Kusini ndio waliosalia kuwania nafasi ya kuandaa mashindano ya 30 na 31 ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilishinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1974, wakati huo ikijulikana Zaire, lakini haijawahi kuandaa mashindano hayo.