Wasiwasi kushirikiana Hispania na Ureno

Shirikisho la mpira wa miguu, FIFA limechapisha taarifa ya kiufundi kuhusu kila nchi iliyojitosa kutaka ipewe fursa ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2018 pamoja na 2022.

Image caption Makao Makuu ya FIFA

Kundi la wachunguzi kutoka FIFA lilitembelea kila nchi iliyojiandikisha kutaka fursa hiyo ili kutathmini uwezo na upungufu walio nao.

Taarifa hiyo imepangwa kuwawezesha wapiga kura kwenye Kamati kuu ya FIFA waweze kutumia vipimo hivyo katika uamuzi wao.

FIFA imechapisha sehemu tu ya uchunguzi wao wa siku nne uliofanywa katika nchi hizo mapema mwaka huu.

Kati ya Mataifa ya Ulaya yanayowania kuandaa fainali ya Kombe la mwaka 2018, England pamoja na maombi ya Hispania na Ureno kuandaa kwa pamoja yameonekana kama yasiyo na upungufu, ingawa England inaonekana kupungukiwa na hoteli na viwanja vya kufanyia mazowezi.

Hispania na Ureno pamoja na maombi ya Uholanzi ikishirikiana na Ubelgiji yamekumbwa na hofu ya ushirika wa kuandaa fainali moja.

Mashaka yamezuka kuhusu vifaa na umbali wa baadhi ya viwanja nchini Urusi ambayo imejinadi kuwa tayari kutoa mabilioni ya dola kwa ujenzi wa viwanja vipya kote nchini.

Kwa upande mwingine hapana wasiwasi juu ya kiwango cha ukiukaji sheria.

Kuhusu kuandaa Kombe la mwaka 2022 shughuli ya kundi la wataalamu imerahisishwa na kuwa maombi ya Qatar yamefuatiwa na onyo kuhusu madhara yanayoweza kusababishwa na joto la kupindukia katika nchi hiyo katika miezi ya Juni na Julai.

Qatar imependekeza kujenga mitambo ya kuondoa joto hilo katika viwanja na vifaa vyote vya michezo wakati wa fainali hizo.

Marekani iliyowekwa juu miongoni mwa nchi zinazoweza kujishindia fursa hiyo imeshutumiwa kutokana na serikali kupuuza ombi lake.

Australia, Korea ya kusini na Japan ni wagombea wengine wa fainali ya mwaka 2022.

Maelezo zaidi kuhusu kila mgombea yamewasilishwa kwa wanachama wa Kamati kuu ya FIFA.

Bado haijafahamika Ripoti hiyo itakuwa na ushawishi wa kiwango gani kwa wapiga kura.

Nchi zote zinazoshiriki kinyanganyiro hicho bado zina fursa moja ya kujitetea mwanzoni mwa mwezi ujao wa Desemba.

Uamuzi wa mwisho utafanywa tarehe 2 Desemba.