Conde achaguliwa rais mpya wa Guinea

Rais mteule wa Guinea
Image caption Rais mteule wa Guinea

Tume ya uchaguzi nchini Guinea, imesema kiongozi wa upinzani nchini humo, Alpha Conde, ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Tume hiyo imesema kuwa Bwana Conde, amepata asilimia 52 ya kura zote zilizohesabiwa.

Uchaguzi huo ndio wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo tangu taifa hilo lijinyakulie uhuru mwaka 1958 na uliandaliwa baada ya miaka miwili ya utawala wa kijeshi.

Matokeo hayo yametangazwa siku moja tu baada ya hali ya taharuki kutanda katika mji mkuu wa Conakry.

Maelfu ya wafuasi wa mpinzani wa Bwana Conde, Cellou Dallein Dialo, waliteketeza magurudumu ya magari huku wakiweka vizuizi kwenye barabara za mji huo.

Lakini Bwana Conde, anasema wakati umewadia kwa wapinzani wake kuungana na kushirikiana naye, ili kuimarisha umoja na utangamano nchini humo.

Duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa urais ilicheleweshwa mara mbili kutokana na makabiliano makali kati ya wafuasi wa Bwana Conde na Diallo, ambao wanatoka makabila mawili makubwa nchini Guinea.