Mamake Ghailani aridhika na uamuzi wa mahakama

Ahmed Ghailani
Image caption Ahmed Ghailani

Mamake Ahmed Ghailani, mshukiwa wa ugaidi ambaye alipatikana na hatia ya kuhusika katika njama ya kulipua balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania, ameelezea kuridhika kwake, na uamuzi wa mahakama wa kutompa mwanawe adhabu ya kifo.

Watu 212 waliuawa mjini Nairobi na wengine 11 mjini Dar es Salaam wakati mabomu yaliyotegwa kwenye balozi za Marekani yalilipuka kwa wakati mmoja.

Mahakama mjini New York ilimpata Ghailani ambaye ni raia wa Tanzania na hatia ya shtaka moja tu kati ya 285.

"Kwanza kabisa nilikuwa na furaha niliposikia kwamba haikuwa hukumu ya kifo," alisema Bi Mkubwa Ghailani alipohojiwa na BBC.

"Nasikia kwamba huenda asipewe kifungo cha maisha, na hilo pia linaniridhisha."

Alielezea matumaini yake kwamba mawakili wanaomtetea Ghailani watafaulu katika jitihada zao za kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Wakili wake Peter Quijano alisema waliamini tangu awali kwamba Ghailani hakuwa na hatia yoyote.

Image caption Ubalozi wa Marekani ulioshambuliwa mwaka wa 1998 mjini Nairobi

Baada ya kupongeza uamuzi huo, alielezea masikitiko yake kwa wale waliofariki dunia katika shambulio hilo: Wakili Quijano alisema kabla ya uamuzi huo kutolewa, Ghailani alionekana kuwa mtulivu.

Aliamini kwamba alikuwa ametendewa haki na hilo pia lilinituliza.

Mtaalum wa maswala ya usalama nchini Kenya Werunga Simiyu, aliikosoa serikali ya Kenya kwa kushindwa kuwakamata waliopanga njama za kulipua mabomu hayo.

Alisema serikali ingefanikiwa katika harakati zake kama ingekuwahusisha raia kikamilifu.

Ghailani alikamatwa nchini Pakistan mwaka wa 2004 na kupelelekwa gerezani Guantanamo Bay.

Kisha alihamishiwa mjini New York mwaka wa 2009 ambako kesi yake imekuwa ikiendeshwa.