Madagascar yamaliza uasi

Madagascar
Image caption wanajeshi walivamia kambi

Wanajeshi wa Madagascar wamevamia kambi ya jeshi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na waasi, na kumaliza siku tatu za uasi.

Milio ya bunduki ilisikika, kabla ya kusikika kwa taarifa kuwa wanajeshi waasi wamejisalimisha na kutiwa mbaroni.

Waasi hao walikuwa wamejificha katika nyumba za jeshi karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Antananarivo, tangu walipotangaza kupindua serikali siku ya Alhamisi.

Baadhi ya waasi walikuwa wanajeshi waliomuweka madarakani Rais Andry Rajoelina mwaka 2009.

Bw Rajoelina ametengwa kidiplomasia, tangu alipoingia madarakani mwezi Machi mwaka 2009, na amepuuza jitihada za wasuluhishi za kutaka kumpatanisha na upande wa upinzani.

Madagascar imekuwa katika mitikisko kwa miaka kadhaa.

Image caption Andre Rajoelina

Mamia ya wanajeshi walionekana wakielekea katika eneo hilo la kambi ya jeshi siku ya Jumamosi, kabla ya taarifa kupatikana za kusikika kwa milio ya bunduki. Hata hivyo mara moja hali iliwekwa chini ya udhibiti, na habari kupatikana kuwa waasi walijisalimisha wenyewe.

"Shughuli imekamilika. Wamejisalimisha wenyewe. Imemalizika bila ya damu kumwagika," amesema Alain Ramaron, mkuu wa baraza la seneti la ulinzi, akizungumza na shirika la habari la AFP.

Akikaririwa na AFP amesema shughuli nzima ya kijeshi imetumia dakika 20.

Image caption Rais Rajoelina

Maafisa wa kijeshi ambao waliasi, walitangaza kufanya mapinduzi, wakati Madagascar ikijiandaa kupiga kura ya maoni ya katiba mpya, ambayo itamruhusu Bw Rajoelina kuongeza muda wake wa urais.

Ikikabiliwa na uasi, serikali siku ya Ijumaa iliwaambia wananchi wanaoishi karibu na kambi ya jeshi, waondoke katika eneo hilo.

Mkuu wa majeshi Jenerali Andre Ndriarijoana, alikwenda kambini hapo kwa ajili ya mazungumzo na maafisa hao waasi, ingawa hakuna taarifa za kutosha zilipatikana kuhusiana na mkutano huo, kabla ya kufanyika kwa matukio ya Jumamosi.

Katiba hiyo mpya ambayo itapigiwa kura ya maoni, itamruhusu Bw Rajoelina kundelea kukaa madarakani mpaka atakapoweza kuandaa uchaguzi.

Image caption Ghasia za mwaka 2009 zilizomuweka madarakani Rajoelina

Pia katiba hiyo itaruhusu umri wa mgombea urais kupunguzwa kutoka miaka 40, hadi 35, na hivyo kumpa nafasi Bw Rajoelina mwenye miaka 36, kuwania nafasi hiyo.

Bw Rajoelina, ambaye amesema hatowania nafasi ya urais, ameandaa mikutano mikubwa ya watu akiwataka kuunga mkono mabadiliko ya katiba.

Rais huyo ambaye aliwahi kuwa DJ na meya wa mji mkuu, alipata umaarufu kufuatia wimbi la watu kumuunga mkono.

Lakini baadhi ya wachambuzi wanasema kushindwa kwake kutatua mizozo ya uongozi, kumepunguza umaarufu wake.

Katika hatua ya kufanyika kwa kura ya maoni, kulikuwa na maandamano ya kupinga hatua hiyo, na vyama vyote vitatu vya upinzani, ambayo vinaongozwa na watu ambao wamewahi kuwa marais wa nchi hiyo wametaka watu kususia kura hiyo.