Hatimaye Arsenal yaondoa nuksi

Arsenal imefanikiwa kuilaza Aston Villa na kwa muda mfupi waliweza kukalia kiti cha Ligi Kuu ya England kwa ushindi wa mabao 4-2.

Image caption Wachezaji wa Arsenal wakishangilia

Andrey Arshavin ndiye aliyekata utepe wa mabao kwa Arsenal kwa mkwaju mkali mbele ya walinzi wa Aston Villa na bao la pili likapachikwa na Samir na Nasri kwa mkwaju wa juu.

Ciaran Clark alirejesha matumaini kwa Aston Villa baada ya kupachika bao kwa mkwaju wa yadi 18, lakini Marouane Chamakh akapangua matumaini hayo ya Villa na kuifungia Arsenal bao la tatu.

Lakini alikuwa Clark tena aliyeweza kupachika bao la pili na kuanza kurejesha matumaini kabla Jack Wilshere katika dakika za nyongeza kufunga bao zuri kwa kichwa cha kuchupia na kuihakikishia Arsenal ushindi.

Kwa ushindi huo Arsenal imefikisha pointi 29, ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Manchester United wenye pointi 31.